Tuesday, 19 August 2014

HABARI ZA KUTWA RASI FM RADIO STATION....SOMA HAPA!!

DODOMA                      

Walimu wa shule ya msingi  Chamwino B manispaa ya Dodoma  wamezitaka mamlaka zinazohusika kufanya ukaguzi wa kina kabla ya kutoa leseni kwa wafanyabiashara wanaoonyesha picha za video kwenye mabanda mitaani.


Wakizungumza  shuleni hapo na kituo hiki walimu hao wamesema kuwa mabanda hayo yanayotumika kuonyesha picha hizo yamezagaa kila mahali bila kujali  athari zinazoweza kujitokeza kwa watoto hasa wanafunzi.

Mwalimu wa shule hiyo Grace Lisasi amesema kuwa wenye dhamana ya kutoa leseni ndiyo wanatakaiwa kufanya uchunguzi na kubainisha nia wapi yanapo stahili kuwekwa mabanda hayo.

Aidha amesema kuwa watu wanao onyesha video hizo hawana huruma na watoto kutokana na kuwarusu kuingia na kutazama picha hizo hata pale wanapo kuwa kama wamevaa sare za shule hali inayosababisha wengi wao kukosa masomo.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi shuleni hapo wamesema ni vyema mwanafunzi mwenyewe akajitambaua na kuacha kuingia kwenye mabanda hayo, kwani wanapoteza muda mwingi wa masomo na kuharibu mwelekeo wa maisha yao.


DAR  ES  SALAAM                       
Baraza la Habari Tanzania (MCT), limetoa  idhini ya kudumu kwa vyuo vitano vya uandishi wa habari nchini kutumia mitaala ya taifa iliyothibitishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Hatua hiyo imefikiwa baada ya MCT kwa kushirikiana na NACTE kufanya ukaguzi wa vyuo hivyo mwaka huu ili kubaini uwezo wao kutumia mitaala hiyo na vigezo muhimu, uwepo wa vifaa, mazingira ya taaluma, miundombinu na uongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, John Mireny,  amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Dar es Salaam School of Journalism, Time School of Journalism na Royal School of Journalism vilivyoko Dar es Salaam. Vingine ni Muslim University cha Morogoro na Teofilo Kisanji cha Mbeya.

Bwana Mireny amesema  kuwa vyuo hivyo vinaongeza idadi na kuwa na vyuo saba vilivyopewa idhini ya kudumu kutumia mitaala hiyo, na vingine viwili vilivyokaguliwa mwaka jana ambavyo Institute of Professional Studies kilichopo Dar es Salaam na Arusha Journalism Training College cha jijini Arusha.

Ameongeza kuwa  vyuo hivyo vitakuwa vinatoa elimu kuanzia cheti hadi diploma huku vyuo vingine vitatu vikiwa tayari vimeruhusiwa kutumia mitaala hiyo kwa muda.

Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Kyela Polytechnic College cha Mbeya, Insitute of Social Media Studies kilichopo Arusha na Morogoro School of Journalism cha Morogoro.

Ameongeza kuwa baraza litafanya mapitio madogo ya mitaala hiyo kuanzia leo ili kufanya maboresho katika maeneo kadhaa  na zoezi hilo litawahusisha walimu kutoka vyuo vya habari na wahariri waandamizi 12.


 
ARUSHA                       

Waziri mkuu mizengo pinda amewataka watendaji mbalimbali wa ngazi ya mkoa na wilaya kuhakikisha kuwa wanakuwa na usimamizi wa karibu ili kuhifadhi miundi mbinu ya barabara ambayo imekuwa ikitumia fedha nyingi za serilali kwa ajili ya utengenezwaji.
Waziri mkuu Ameyaseama hayo wakati akifungua mkutano wa wadau wa barabara za halmashauri uliofanyika Jijini Arusha wenye lengo la kutathimini matatizo mbalimbali yanayokabili miundo mbinu ikiwemo ya barabara za halmashauri nchini.
Kwa  upande wao wadau wa mfuko  wa barabara akiwemo waziri wa TAMISEMI Mheshiwa Hawa Ghasia amesema kuwa zipo changamoto zinazokabili utekelezaji wa barabara huku wakitaka uanzishwajiwa wa wakala wa usimamizi wa barabara utakaokuwa chini ya halimashauri.

Wamesema kuwa endapo miundo mbinu ya barabara hasa za vijijini haitarekebishwa itakuwa ni vigumu kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo wajumbe kutoka halimashauri ya wilaya ya Arusha wamesema kuwa katika mwaka wa fedha uliopita waliweza kutenga fedha katika mapato ya ndani na kununua mitambo mbalimbali ambavyo vilifanikisha kufanya uboreshaji wa barabara hali iliyopelekea kuwa halmashauri ya kwanza nchini kutokana  na ununuzi wa vifaa hivyo.




DODOMA                   

Wafanyabiashara wa soko  kuu la majengo manispa ya Dodoma wameiomba serikali kufungua masoko ya nje ili kuyanusuru mazao ambayo yameshuka bei kwa kiasi kikubwa.
Mmoja wa wafanyabiashara hao Bwana Said Kimolo ameiambia Rasi FM kuwa soko la  mazao limeshuka kwa kiasi kikubwa kutokana na masoko ya nje kufungwa.
Mfanyabiashara huyo amesema mpaka sasa hawaelewi mpango wa serikali nini kuhusiana na soko la nje kuwasaidia ili wapate soko la kuyapeleka mazao yaliyojaa  sokoni hapo.
Amesema mji wa Dodoma uko chini sana kibiashara hivyo serikali badala ya kukaza kuendelea kukusanya kodi ni vizuri pia wakaangalia namna ya kuwasaidia kufungua soko la nje ili waweze kuuza mazao waliyonayo.
Aidha amesema  kuwa kingine kinachochangia upungufu wa mauzo sokoni hapo ni vyuo vikuu vilivyopo mkoani hapa kufungwa kwa wakati mmoja tena kwa muda mrefu wa miezi mitatu.


DAR  ES  SALAAM               
Serikali imesema kuwa haipo tayari kufunga mipaka yake kwa sasa kuzuia wananchi wa nchi zinazo kabiliwa na ugonjwa wa ebola kuingia nchini.

Kauli hiyo imetolewa  jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dokta Seif Rashidi, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Kwa sasa ugonjwa wa ebola umezitikisa nchi kadhaa za Afrika Magharibi huku ikiripotiwa kuwa takribani watu zaidi ya 400 nchini Liberia wamefariki Dunia  huku watu zaidi ya 1,000 wamepoteza maisha.
 
Waziri Rashidi amesema  ili kufikia hatua hiyo ya kufunga mipaka ni lazima kuwa na makubaliano katika  kanda husika na ushauri kutoka Shirika la Afya Duniani juu ya hatari inayoweza kutokea kwa nchi husika.

Wakati huo Shirika la Ndege la Kenya limesitisha safari za ndege la shirika hilo kuelekea mataifa matatu yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa na mlipuko wa ugonjwa wa ebola. 

Kenya imesema kuwa baada ya kupata ushauri wa WHO na Wizara ya Afya  ya nchini Kenya, shirika hilo limeamua kusimamisha safari zote za ndege kwenda Liberia na Sierra Leone.

CAIRO               
Kiongozi  wa  ujumbe  wa  Wapalestina  katika majadiliano ya  amani  na  Israel  amesema kuwa  ghasia zinaweza  kuzuka  tena katka Ukanda  wa  Gaza,  iwapo hakuna hatua zinazopigwa kuelekea  makubaliano  ya kudumu.

Wajumbe  wa  majadiliano  wa  Israel  na Palestina  wamerefusha  usitishaji  mapigano, kwa  lengo la  kuendeleza  mazungumzo ya  kumaliza  mashambulizi dhidi ya Ukanda  wa  Gaza.

Hata  hivyo  kiongozi  wa ujumbe  wa  Palestina Azzam al-Ahmad, amewaambia waandishi  habari  mjini  Cairo  kuwa  hakuna  hatua zilizopigwa kuhusu  kipengele  chochote  katika mazungumzo  hayo, na  kwamba  ghasia  huenda zikazuka  tena kabla  ya  muda  mpya  uliowekwa  wa kusitisha  mapigano kumalizika. 


JOHANNESBURG                
Watu 9 wamefariki Dunia baada ya kuangukiwa na nyumba katika eneo la Alberton  mjini Johannesburg.

Msemaji wa shirika la huduma ya kwanza Bwana William Ntladi amesema Idadi hiyo huenda ikaongezeka kwa kuwa baadhi ya watu bado wamekwama kwenye kifusi cha nyumba hiyo.

Timu ya uokoaji inaendelea kufanya juhudi kuwatafuta walionusurika. Hadi sasa chanzo za kuporomoka kwa jengo hilo bado hakijajulikana.


KIEV                         
 Msemaji  wa wizara  ya mambo ya kigeni ya Ukraine amesema  kuwa  Kansela Angela  Merkel wa  Ujerumani atasafiri  kwenda  mjini  Kiev siku  ya  Jumamosi  kwa mazungumzo  ya  kisiasa  kuhusu mzozo  wa  Ukraine.
Ziara  hiyo  itafanyika  katika  mkesha  wa  sherehe  za uhuru  wa  Ukraine.

Wakati  huo   miili ya watu 15 imepatikana  hadi  sasa  kutoka eneo lililoshambuliwa  kwa  roketi  Agost 18 mwaka huu  dhidi  ya msafara wa  mabasi  na  magari  madogo  ya  wakimbizi mashariki  mwa  Ukraine.

Shambulio  hilo  lilitokea  karibu na  mji  wa  Luhansk, karibu  na  mpaka  wa  Urusi katika eneo  ambalo  kumekuwa  na  mapigano  makali  kati  ya majeshi  ya  serikali  na  wapiganaji  wanaotaka  kujitenga wanaounga  mkono  Urusi.


Jeshi  la  Ukraine  limewalaumu wapiganaji,  na  wao  wamekana  kuhusika  na  shambulio hilo.

No comments:

Post a Comment