DODOMA
19.08.2014
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu
ya CCM inakutana leo mchana mjini Dodoma chini ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya
Kikwete huku ikitarajiwa kufanya uamuzi mgumu wa mchakato wa Katiba.
Kikao hicho kinakutana kwa
mara ya pili katika muda mfupi, baada ya hivi karibuni kukaa jijini Dar es Salaam kikiwa na lengo la
kujadili mchakato wa Katiba unaoendelea
Akizungumzia kikao hicho,
mtaalamu wa sayansi ya siasa na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dokta
Alexander Makulilo amesema jambo kubwa litakalojadiliwa katika kikao hicho ni
kauli tofauti zilizotolewa na wananchi kuhusu mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Duru za habari zinadai kuwa kikao hicho kinaweza kupendekeza
kuwashughulikia wanachama wake waliotoa kauli zinazopingana na msimamo wa chama
hicho.
MWISHO.
KILIMANJARO
19.08.2014
Jamii imeshauriwa kuchukua tahadhari kwa kunawa
mikono kabla na baada ya kula ili kuweza kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya
milipuko.
Ushauri huo umetolewa na Ofisa Afya Mratibu wa
Kampeni ya Usafi wa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani
Kilimanjaro Bibi Joyce Tarimo wakati
akizungumza na wakuu wa Shule, waratibu elimu , wenyeviti wa bodi za shule, na
wenyeviti wa viijiji iliyolenga utekelezaji wa mikakati ya taifa ya kampeni ya
usafi iliyofanyika kwenye ukumbi wa kanisa katoliki wilayani Siha.
Awali akitoa mada katika Semina hiyo Afisa wa
Kitengo cha Afya na Mazingira Wilayani siha Lidya Joseph amewataka viongozi
kusaidia kuelimisha jamii namna ya kujikinga na Maradhi hayo.
Nae Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo Bwana Rashidi
Kitambulio amewataka viongozi hao kuacha tabia ya kutoa maagizo badala yake
watumie muda mwingi kuielimisha jamii madhara ya uchafu .
Hata hivyo Bwana Kitambulio amesema Serikali imejipanga
vyema kuhakikisha maradhi hayo hayasambai ,kwa kutoa elimu mbalimbali sambamba
na kuendesha vipindi vya dharura kwa jamii ili kupunguza maradhi hayo.
MWISHO.
DAR ES SALAAM
19.08.2014
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam limetumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu wenye ulemavu wa
ngozi (albino), waliokuwa wakizuia gari la polisi lililokuwa limebeba mtuhumiwa
wa kutishia kuua Albino kwa maneno.
Tukio hilo limetokea jijini
Dar es Salaam ambapo walemavu wa ngozi hao wamevamia gari hilo na kuwataka
askari polisi wamshushe ndani ya gari mtuhumiwa huyo aliyetambulika kwa jina la
Ombeni Michael, ili wafahamu alipokuwa akipelekwa.
Vurugu hizo zilianza katika
Mahakama ya Mwanzo Buguruni, ambapo walemavu hao walivamia wakati kesi
dhidi ya mtuhumiwa huyo ikiendelea katika mahakama hiyo.
Baada ya kusikilizwa kwa kesi
hiyo na dhamana kuwa wazi kwa mujibu wa sheria, watu hao wenye ulemavu
waliamsha hasira ya kupinga kupewa dhamana kwa mtuhumiwa huyo.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi
Septemba 3, mwaka huu.
Aidha Mwekahazina wa Chama cha
Albino Tanzania, Abdillah Omary, alilazimika kuandika barua mahakamani hapo
kupinga hatua ya kupewa dhamana kwa mtuhumiwa huyo.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya
Ilala, Mary Nzuki, amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo, huku akisema kuwa
hali hiyo imechangiwa na mwili wa mwanamme mmoja aliyedhaniwa ni mlemavu wa
ngozi kuokotwa amefariki dunia Tabata Kinyerezi mwishoni mwa wiki iliyopita.
MWISHO.
DODOMA 19.08.2014
Wakazi wanaopitiwa na mradi wa umeme
wa vijijini (Rea) Mkoani Dodoma wamelalamika kufanyiwa vitendo vya utapeli
vinavyofanywa na watu wanaofahamika kama vishoka.
Akizungumza na kituo hiki mmoja wa
wakazi wa kijiji cha Makoja Wilayani Chamwino Bwana Matonya Msena amesema vishoka
hao wamekuwa wakipita nyumba hadi nyumba na kuwatoza michango ya kusaidia
kuwaunganishia umeme Kwa gharama ya shilingi laki moja hadi laki tatu wakati
gharama halisi za kuunganisha nishati hiyo ni shilingi elfu thelatihini na
mbili na mia tisa tu.
Amesema kutokana na tabia hiyo ambayo
tayari wakazi wengi wameshatapeliwa fedha zao kwa vishoka hao,wameliomba
shirika la Tanesco kutoa elimu kwa wananchi ili kuweza kuwatambua wahalifu hao.
Amesema elimu hiyo pia itaweza
kusaidia hata kuwachukulia hatua za kisheria pindi watakapokamatwa hao vishoka
ili kukomesha tabia hiyo.
Kwa upande wao Afisa masoko wa
shirika la Tanesco Makao Makuu Bibi Jennifer
Mgendi na Mhandisi afya na usalama Tanesco Athanas Zawadi Wamesema mradi wa
umeme vijijini Rea Mkoani Dodoma umeanza kutekelezwa kuanzia mwezi january
mwaka 2014 na unatarajiwa kukamilika ifikapo june 2015, kwa gharama ya zaidi ya
shilingi bilioni 54 huku wakazi wa vijiji vinavyopitiwa na mradi huo wakiwa na
matarajio makubwa ya kujikwamua kiuchumi.
MWISHO.
NAIROBI 19.08.2014
Kampuni
ya ujenzi ya China imesema imewaajiri wakenya wapatao 2,464 kwa ajili ya kazi
ya mwanzo ya mradi wa kujenga reli unaotarajiwa kurahisisha usafirishaji wa
bidhaa nchini humo.
Akizungumza
mjini Nairobi baada ya kufanya mazungumzo na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, mwenyekiti msaidizi wa kampuni ya ujenzi ya
China, Bwana Wen Gang, amesema kampuni
yake itatoa ujuzi na kuwapeleka watu wa
Kenya ili kusaidia nchi katika utengenezaji wa vifaa vya mradi huo wa ujenzi.
Amesema hadi mwishoni mwa mradi huo, zaidi ya
wakenya 30,000 watakuwa wameajiriwa moja kwa moja na asilimia 40 ya kazi
zitakwenda kwa makampuni ya Kenya.
Wakati
wa mkutano huo rais Kenyatta amepongeza ahadi za kampuni hiyo za kushirikiana
na wenyeji ili kusukuma mbele kiwanda cha utengenezaji chuma nchini humo.
Reli
hiyo inalenga kutoa ufanisi na gharama nafuu za usafiri wa reli kwa mizigo na
abiria.
MWISHO.
WASHINGTON 19.08.2014
Rais wa Marekani Barack Obama amesema majeshi
ya Iraq na yale ya Kikurd yamepiga hatua kubwa kulitwaa tena bwawa muhimu la
Mosul kutoka kwa wapiganaji wa kiislamu kaskazini mwa Iraq.
Amesema
wamethibitisha kwamba wanauwezo wa kufanya kazi kwa pamoja na wataendelea
kuungwa mkono na majeshi ya Marekani, ambayo tayari yamefanya mashambulio Zaidi
ya anga katika eneo linalokaliwa na wapiganaji wa kiislamu.
Ripoti
zinasema kuwa mapambano katika juhudi za kudhibiti maeneo yanayozunguka bwawa
hilo yanaendelea.
Katika
hatua nyingine kundi la himaya ya kiislamu linalofanya mashambulizi dhidi ya
Wakurd limekanusha kwamba wapiganaji wake wamepoteza udhibiti wa bwawa hilo.
Wakati
huohuo kiongozi wa kanisa katoliki duniani papa Francis amesema jumuiya ya
kimataifa itakuwa na haki katika kuchukua hatua dhidi ya wanamgambo hao.Amesema
ni halali kuzuia kile alichokiita dhuluma ya kichokozi.
MWISHO.
SIOL 19.08.2014
Tangu kuanza kwa ugonjwa wa
Ebola kumekuwapo na malalamiko ya watu wanaotoka Barani Afrika kutengwa kwa
kutopewa huduma za kijamii nchini Korea kusini ikiwamo kutoruhusiwa kuingia katika
Migahawa na usafiri wa umma kwa madai ya kuwa huenda wana virusi vya Ebola.
Aidha, baadhi yao wamedai watu
weusi wanaposimamisha TAXI hazisimami kutokana na hofu ya virusi hivyo vya
Ebola.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment